Jumatano 28 Oktoba 2026 - 18:40
Jumuiya ya Wanazuoni wa Yemen/ Al-Azhar Inasema Uongo

Hawza/ Jumuiya ya Wanazuoni wa Yemen imelaani taarifa ya Sheikh Mkuu wa Al-Azhar kuhusu kushambuliwa maeneo matakatifu ya Kiislamu, na kuielezea kuwa ina “tuhuma kubwa, uzushi wa wazi na ushahidi wa uongo” dhidi ya wananchi wa Yemen, Jumuiya hiyo imetaka taarifa hiyo iondolewe.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Jumuiya ya Wanazuoni wa Yemen imelaani yaliyotajwa katika taarifa ya Sheikh Mkuu wa Al-Azhar kuhusu kushambuliwa maeneo matakatifu ya Kiislamu. Jumuiya hiyo imesema kuwa; taarifa hiyo ina “tuhuma kubwa, uzushi wa wazi na ushahidi wa uongo” dhidi ya wananchi wa Yemen. Aidha, jumuiya hiyo imeeleza kushangazwa kwake na hatua ya taarifa hiyo kukubali madai kwamba Yemen inalenga maeneo matakatifu ya Kiislamu.

Katika taarifa yake, jumuiya hiyo imesema: “Ingelikuwa bora zaidi kwa Sheikh Mkuu wa Al-Azhar kuishauri serikali ya Saudi Arabia na kuitaka isimamishe uchokozi na mzingiro dhidi ya Yemen, badala ya kukubali madai yake ya uzushi.”

Jumuiya ya Wanazuoni wa Yemen imeitaka Al-Azhar kuiondoa taarifa hiyo ili iweze kujiondolea uwajibikaji mbele ya Mwenyezi Mungu. Hii ni kwa sababu, kabla ya kutolewa taarifa hiyo, suala hilo halikufanyiwa uchunguzi, wala hakuna mawasiliano yaliyofanywa na Sana'a ili kusikiliza mtazamo wa upande wa Yemen.

Vilevile, jumuiya hiyo imehoji msimamo unaochukuliwa kuhusu mauaji yanayotekelezwa na serikali ya Saudi Arabia na mashambulizi dhidi ya miundombinu ya kiraia nchini Yemen, imeongeza kuwa matukio hayo yanapaswa kulaaniwa na wahusika wawajibishwe, badala ya wananchi wa Yemen kufanyiwa kampeni za tuhuma.

Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa; serikali ya Saudi Arabia inajaribu kuzihusisha nchi za Kiislamu na wanazuoni wake katika mzozo huu, na kutumia maeneo matakatifu ya Kiislamu ili kuleta uchokozi na mzingiro dhidi ya Yemen sura ya kidini na ya kuchochea fitna.

Jumuiya hiyo, ikirejelea ukweli kwamba uchokozi dhidi ya Yemen ulitangazwa kutoka Washington, imesisitiza kuwa shambulizi hilo ni sehemu ya mpango wa Marekani na Uzayuni, ambao lengo lake ni kudhoofisha uwezo wa Umma wa Kiislamu na kuliandaa eneo hilo kwa ajili ya kile kinachoitwa “Mradi wa Israel Kubwa.”

Mwisho wa taarifa yake, Jumuiya ya Wanazuoni wa Yemen imesisitiza kuwa; wananchi na uongozi wa Yemen wanakaribisha kila juhudi ya Kiislamu inayolenga kutatua tofauti na kuleta maridhiano baina ya pande zinazohusika. Hata hivyo, imeweka sharti kwamba juhudi hizo ziwe na lengo la kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na kutekeleza haki, badala ya kutumikia maslahi ya Marekani na serikali ya Kizayuni.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha